KISA CHA KIHINDI.
Aliondokea Sultani wa Kihindi, akazaa mtoto mmoja, akimpenda sana. Hatta alipokufa, akaagiza mawaziri yake, ufalume mpeni mwanangu, naye mmpende sana, kana mimi. Akafa.
Wakaondoka matanga, akatawala mtoto. Na waziri ana mtoto wake, wakipendana sana wale vijana, wakatumia mali siku nyingi, wakatumia na ufalme.
Hatta siku moja, mtoto wa Sultani akamwambia mtoto wa waziri, na tusafiri, tukaangalie miji. Akamwambia, haya. Wakafanya marikabu, ikapakia vyakula, na fetha, na askari, wakasafiri.
Hatta baharini wakavunja, wakafa watu katháwakatha. Mtoto wa waziri akaliwa na papa, na yule mtumwa wake mmoja akachukuliwa kwa maji. Akapona yeye mtoto wa Sultani, na mtumwa wake mmoja. Wakaangukia mji mgeni.
Walipofika mjini wakakaa mashamba. Yule mtoto wa Sultani akamwambia mtumwa wake; enenda mjini, katafute vyakula, tuje tule.
Alipofika mjini kuna machezo, wamekusanyika watu wangi. Sultani wa mji ule amekufa, wanatafuta Sultani mgine ku'mweka. Hutupa ndimu itakayempiga marra tatu ndiye Sultani.