Page:Swahili tales.djvu/198

This page has been proofread.
178
MOHAMMADI MTEPETEVU.

machoni pangu, kwani mwanangu nimempenda, namwonea uchungu, bassi nisitake kukuthuru.

Aliponiambia vile, nikaona ndiyo yalio. Nikaondoka nikaenda nyumbani kwangu, nikakaa kitako nikawaza, nikatafakari, nikaona nyumba hainiweki, nikatoka kwenda mtafuta mke wangu. Nikaenda wala sijui niende api. Nikalemea njia, nikafuata msitu.

Nikaona nyoka wawili mweupe na mweusi. Na mweusi yule akaja na kinwa wazi anamfukuza yule mweupe. Nikaondoka mimi, nikampiga nyoka mweusi, nikamwua. Yule mweupe akatoka akaenda zake. Akaenda nikamwona akirejea na nyoka watatu weupe kana yeye. Wakamshika yule nyoka mweusi, wakamkatakata vypande vidogo vidogo, wakaisha wakavitupa. Wakaniambia, jamala yako haipotei.

Wakaniuliza, weye siye Mohammadi mtepetevu? Nikawaambia, mimi ndiye mtepetevu? Wakaniambia tena, jamala yako haipotei, nawe twalijua liliokutoa kwenu. Sababu ni mwanamke binti Sherifu, naye mwanamke huyu zamani Maridi yule akitaka kumwiba. Naye yule si nyani, ni Jini, na yale yaliokwambia yakuwa kuna khazina, si khazina, vile na vifungo alivyofungwa yeye, akageuzwa kwa nyani na Sherifu. Na sasa, wakaniambia, inshallah utampata mkeo.

Akaenda akarudi na mtu mmoja mkubwa mno ajabu. Akamwuliza, fullani wamjua? Na fullani huyu ndiye Maridi yule aliokuwa nyani. Akamwambia, namjua, na sasa amegeuka amekuwa hali yake ya kwanza na manamke amempata amemchukua aliyekuwa akimngojea. Na sasa amekwenda yuko mji wa Nuhás. Ameona ulimwengu wote hau'mweki.