Page:Swahili tales.djvu/218

This page has been proofread.

SULTANI MAJINUNI.

Sultani Majinuni alioa mke, binti amu yake, akazaa naye mtoto wa kwanza mwanamume, akazaa naye na mtoto wa pili mwanamume, akazaa naye na mtoto wa tatu mwanamume, akazaa na mtoto wa nne mwanamume, akazaa naye na mtoto wa tano mwanamume, akazaa naye na mtoto wa sita mwanamume, akazaliwa mtoto wa saba kitinda mimba mwanamume. Sultani akafurahi sana kwa kupata simba wale.

Akakaa Sultani, akafanya bustani kuu, akapanda matunda yote ya ulimwengu ayajuaye yeye, naye asiyoyajua akauliza kwa watu akapata, akapanda. Akapanda na mtende moja, akapanda na jamii ya mbogamboga, killa siku aliyakwenda katika bustani marra tatu, aliyakwenda saa ya kwanza, akaenda na saa tissia, akaenda na saa edhashara u nussu.

Sultani akakaa na watoto wake, akawatia chuoni, wakasoma wakaihtimu wakafundishwa barua, wakajua.

Bassi katika watoto wale, yule wa saba, baba yake hampendi. Kazi yake yule mtoto hatoki jichoni kwa waanaake, hatoki katika chini ya vinu kwa waanaake. Akakasirika sana baba yake sababu yule kukaa kwa waanaake.