mkeo sina uso kwa watu. Killa nitakapokwenda, katika ukumbi wa watu, sitaweza kuinua uso wangu kutazama watu pia, wake kwa waume, wangwana kwa watumwa, wadogo kwa wakubwa, wataniambia mimi kama nimezaa kwa haramu. Bassi wewe, Bwana, wapenda niambiwe maneno kama hayo na watu? Akamwambia, hasha, sipendi mimi waambiwe maneno mabaya na watu, licha ya haya hatta mangine mabaya, sipendi waambiwe na watu. Napenda mimi nikupe maneno mema na wote watu watakaosikia katika inchi hii ao inchi nyingine, wakiambiwa kama Sultani Majnuni humpa maneno matamu mkewe, hamkasiri mkewe, lile atakalo mkewe ndilo amfanyalo, na watu wangine watakufanya kama yale. Akamwambia, ahsanti, bwana wangu, ndilo jambo nalilotaka kwako, nami nimelipata. Na vijana na vikae kitako.
Bassi yule kijana kitinda mimba, akipendwa sana na babaye, na bibi akimpenda sana, na shangazi lake akimpenda sana na mjumba wake akimpenda sana, kuliko wale nduguze watu sita. Wale watu sita walikipendwa sana na mama yao, kuliko yule kitinda mimba. Yule mke akamwambia mumewe, siachi wingi kwa uchache, siachi waana sita hampenda mmoja.
Bassi wakakaa kitako, hatta yule paka wa Sultani akaenda akakamata ndama wa ng'ombe. Akaenda akaambiwa Sultani yule, paka amekamata ndama wa ng'ombe, akawaambia, paka wangu na ndama wangu. Wakamwambia, vema, bwana.
Wakakaa baada ya siku mbili tatu, akakamata koo la mbuzi. Wakamwambia, Bwana, paka amekamata koo la mbuzi leo. Akamwambia mbuzi wangu na paka wangu.
Wakakaa baada ya siku mbili, akakamata ng'ombe. Akaenda akaambiwa, bwana, paka amekamata ng'ombe. Akawaambia, ng'ombe wangu na paka wangu.