Page:Swahili tales.djvu/356

This page has been proofread.
336
HASSIBU KARIM AD DINI.

jiwe, akagonga chini, akasikia panalia wazi. Akawaita wenziwe, akawaambia, hapa panalia wazi!

Wakamwambia, gonga, akagonga, wakasikia panalia wazi, wakamwambia, tuchimbe. Wakachimba, wakaona shimo kubwa, limekaa kana kisima, wakaangalia ndani mna asali, limejaa tele.

Wakaacha kuni, ikawa kuchukua asali, kulla siku. Na yule Hassibu ndiye, aliyeliona mbele ile shimo la asali. Wakamwambia, wewe ingia mmo ndani, ukiteka asali, ukatupe sisi, tukaende tukauze mjini, hatta tukiisha, tupate kugawanya fetha. Akanena, vema.

Ikawa kazi zao kulla siku miezi mitatu, wakapata mali mengi.

Hatta asali ilipokwisha, imesalia chini kabisa nako mbali, wakamwambia, ingia wewe ndani kule, ukwangue iliosalia chini, ukiisha, tutakupa kamba, ushike, tukupandishe juu. Yule akakubali, akakusanya, akawaambia, nipeni kamba. Wakamwambia, hapana kamba, ngoja kwanza, inakuja. Wakafanya shauri, wakasema, huyu na tumwache mumo humo ndani ya shimo, tugawanye sisi mali.

Akaondoka mmoja, akasema, mama yake, tutamwambiaje? Akaondoka mmoja, akajibu, akamwambia, tutamwambia, mtoto wako aliondoka, kwenda chooni, akakamatwa na simba, yeye na punda wake, nako ndani ya mwitu tusiweze kumtafuta sana, lakini tukasikia simba analia, tukajua aliyemkamata ni yeye simba.

Wakaenda zao mjini, wakamwambia mamaye. Mamaye akalia sana, akakaa matanga, hatta yakaisha. Wale wakagawanya fetha, wakasema, tumpelekee na mama ya rafiki yetu kidogo fetha, wakampelekea. Bassi kulla