Sha'iri la Makunganya
"Sha'iri la Makunganya"; mwenye kuandika Mzee bin 'Ali bin Kidogo bin il-Qadiri, Zanzibar
1-6
- Bismillahi awali,
- ya pili rahmani
- nataka kutakallam,
- na khabari kwapani
- msishikwe na ghururi,
- tafaddalini jamani
7—12
- na shamba mtapandiwa
- leo mnajuta nini
- baa la kujitakia?
- bass mwalimkisema
- ashukapo Jerumani
13-19
- Tutapigana jihadi
- Kwa rehema ya mannani,
- Jeremani akashuka
- Akangia fordani.
- Pasiwe mtu kujibu
- Ikawa kutaka amani,
- Leo mnajuta nini
20-26
- Baa la kujitakia?
- Mtawambia kwa yaqini
- Niwape yangu moyoni
- Nitasema kwa baini
- Waliondoka mjini
- Waliokwenda utamboni
- Kilwa Kivinje mjini.
27-32
- Ntawataja fursani
- Waume wanao shani
- Waliondoka mjini
- Wakaingia sitimani
- Watoto wa Kijerumani.
- Ma'askari yaqini
33-38
- Elfu na sabini:
- Kuwataja sitaweza
- Watu wote kujitengeza:
- Amiri jeshi Raamza,
- Ndiye aliye haziria.
- Leo mnajuta nini?
39-45
- Baa la kujitakia?
- Wazungu thabiti mitima yao
- Yalikuwa marudia.
- Wala haina khofu
- Kulla harubu kuingia
- Na furaha kuwapata,
- Shindo wakilisikia,
46-52
- Na bunduki mikononi
- Mji wakuwania.
- Leo mnajuta nini,
- Baa la kujitakia?
- Kwa kulla neno ntatia
- Hapana lakubaqia:
- Khabari ya Makunganya.
53-58
- Sikizeni ntawambia:
- Alianza upotovu
- Kufanya mambo daifu
- Na watu kuta'arifa
- Kujifanya mtukufu,
- kumbe kijitu daifu
59-64
- Machoni ukimtokea;
- Wenziwe akawaghuri
- Pasiwe kufikiri;
- Wakaingiwa na ghururi
- Wakaja wakafa zuri
- Hatta shahada kutoa.
65-72
- Ukali wake kama ra'adi
- Jerimani; hawarudi.
- Huenenda kama jaradi
- Hapo watapotokea.
- Askari wa Jermani
- Anavowapamba kwa shani
- Viatu viko miguuni
- Na mabete kiunoni
73-80
- Burangiti mgongoni
- Gisi wanavowalia
- Leo mnajuta nini,
- Baa la kujitakia?
- Walipoazim vita
- Kwa Makunganya kufika
- Hatta walipomshika
- Na watu kumi na sita:
81-89
- Hapana pakutokea
- Ote wakatiwa nyororo
- Wakawa kama watoro
- Zikawafa roho zao
- Nafsi zao kupotea.
- Watu waliposhikana
- Vita vilipopigana
- Mjini mwa Makunganya
- Watu kujikimbilia
90-98
- Watumwa kwa wangwana;
- Hapana mtu kusema
- Wote wana teketea
- Watu wa Makunganya
- Wamekufa kama panya
- Gisi alivoingiliwa.
- Boma lake likavunjwa
- Watu yake wakanyongwa
- Wakewe wakapotea
99-106
- Naye tanzini kangia.
- Leo mnajuta nini,
- Baa la kujitakia?
- Kwa hesabu sitawesha
- Wengine nitawabaqisha
- Wote wakapigwa picha
- Pasiwe kusalia,
- Leo mnajuta nini,
107-114
- Baa la kujitakia?
- Khabari nitawapani
- Walio ondoka mjini
- Ma'adwi wa zamani
- Waliokwenda Kilwa Kishwani
- Kumondoa Sulutani
- Yeye bwana Vismani
- Na tena na Govmani.
115-121
- Sitima iko tayari
- Imekwisha jingilia
- Wakenda wasimwone.
- Maneno yao wasiseme
- Wakawa kama wagane
- Hapa walipo kukaa.
- Damiri yao moyoni
122-128
- Wampate Vismani
- Bana mkubwa wa shani
- Aqili nyingi kichwani
- Mtoto wa Kijermani
- Ememiliki Kivinji
- Hatta Kilwa Kishwani
- Tangu awali ya Lindi
129-136
- Hatta Tanga Afrikani.
- Leo mnajuta nini,
- Baa la kujitakia?
- Ushahidi sijatoa
- Sasa mnawayawaya - ;
- Bandari Salama Ulaia
- Uzuri wamebarabara
- Jinsi ilivotulia.
137-144
- Zimekwisha sifa zake
- Visman peke yake
- Wala hana mwenzi wake
- Ambaye kumzidia.
- Kwa kulla neno ntatia
- Ni kama hapa Afrika
- Wala hana mushirika
- Sikizeni ntawambia:
145-153
- Leo mnajuta nini,
- Baa la kujitakia?
- Yeye mtu taratibu
- Hakuumbwa na ghadabu
- Ukimwona mwarabu
- Machoni mtokea;
- Ameumbwa na rehema
- Amefanya mambo mema
- Inchi zote kutengea
154-162
- Ajua sana kusema
- Kiswahili kumwelea.
- Leo mnajuta nini,
- Baa la kujitakia?
- Niwacheni nimsifu
- Na yeye mtu nadifu
- Na la tatu mtukufu
- Roho yake hana khofu.
- Tena mtu shuja'a
163-170
- Jina lake tulijua:
- Tangu pwani hatta bara
- Hapo asiyo sikia.
- Leo mnajuta nini,
- Baa la kujitakia?
- Kaipanda Afirika
- Tangu nyanza hatta nyika
- Hapana asipofika
171-178
- Barra yote kutembea.
- Amezaliwa Berlina
- Vismani mtu mwema
- Anaye nyingi rehema
- Watu wote wamjua
- Khabari hio kufika,
- Walipotaka kumshika
- Mwaka u nussu kupita,
179-187
- Hatta siku zikipita
- Shauri akafanyiza
- Na zana akatengeza;
- Wakenda wakifunza.
- Leo mnajuta nini,
- Baa la kujitakia?
- Ushairi ntasema sana
- Siku waliokutana
- Visman na Makunganya.
188-196
- Kwanza alimtukana
- Na yeye kajinamia
- Kumtukana machoni kwake
- Makunganya na watu wake
- Kamwambia: mwanamke.
- Nani anayo kujua?
- Akisema akapoa
- Kitini kajikalia
- Kaondoka bana Mayoa
197-204
- Maneno akitongoa
- Kizungu: hayakumwelea.
- Nitawaambia kwa yaqini
- Sahha na bana Feltini
- Wakasema Kiswahili
- Watu wote kusikia:
- Bana Sahha kamwambia
- Leo mnajuta nini,
205-212
- Baa la kujitakia?
- Banyani na Wahindi
- Waarabu na Washihiri
- Na wengine Waswahili
- Wote wakaitikia.
- Makunganya asiseme
- Wakanyongwa watu saba
- Na mwenyewe ndio wa nane,
213-221
- Hapo asiotazama;
- Watumwa na wangwana
- Wakubwa hatta vijana
- Wote wakashuhudia:
- Leo mnajuta nini,
- Baa la kujitakia?
- Sahha ni bana mzuri
- Wahindi akawashauri
- Wote wakajikania.
222-230
- Bana Sahha akafikiri
- Aqili ikamwingia
- Roho ikaghadhabika
- Karakoni akafika
- Askari akaweta
- Wote wakamtokea;
- Walingiwa na uchungu
- Askari na wazungu
- Wote wakamwandamia.
231-238
- Akafanyiza nadhari
- Akaweka watu wawili
- Mzungu na Asikari
- Nyumba moja kumngojea;
- Maneno nitawakifu
- Zikesha zote nyumba tatu
- Na ya nnne ntawambia
- Nyumba iliobaqia
239-246
- Na jina utawatajia
- Ya Muhindi Kassum Pira
- Bana Sahha akaondoka
- Ile nyumba akangia
- Vitabu akavichukua
- Mfukoni akavitia.
- Akawashauri sana:
- Wahindi wanne wakakana,
247-254
- Bana Sahha akitongoa
- Vitabu akavitoa:
- Ote wakujinamia.
- Leo mnajuta nini,
- Baa la kujitakia?
- Twamjua ma'alum
- Bana Sahha kwa hukum
- Hukumu anaiweza
255-292
- Shauri kuitengeza;
- Naye kawatoza fedha
- Wahindi kujitolea.
- Na Wahindi Kilwa wengi
- Wakatoa fedha nyingi.
- Nitafanyiza hesabu
- Halafu ntawambia:
- Najua kwa yaqini
263-269
- Ni elfu 'asherini
- Hesabu nawambia
- Ni watajiri mbali-mbali.
- Niwasifu mahodari:
- Abdallah bin Omari;
- Ndiye aliyetokea,
- Hakukaa mwanamke,
270-276
- Hakungojea ashikwe,
- Mwenyewe alijiendea
- Hatta tanzini kufika
- Na shingo akaipeleka
- Na tanzi akajitia
- Na watu kumtazama
- Naye kimya hakusema
277-284
- Marra akajangukia
- Khabari nisha wapani
- Ote meshasikia
- Ya Makunganya kuuwawa
- Miji yote wamejua
- Mwanzo hatta akhiria:
- Leo mnajuta nini,
- Baa la kujitakia?
285-292
- Wahindi wakatiwa nyororoni
- Wakawekwa karakoni
- Sitima wakangojea,
- Ilipokuja wakapakiwa
- Wote safiria.
- Wakafika Bender-Essalama
- Wote wkaonekana
- Watumwa kwa wangwana
293-300
- Wote wakatazama
- Hapana asiwaone:
- Wakashukwa kama watumwa
- Kette ilivowangia.
- Leo mnajuta nini,
- Baa la kujitakia?
- Bana Sahha twamjua ma'alumu
- Ajua sana hukumu
301-308
- Kawafunga kwa siku zake
- Aijua miaka yake,
- Halafu atawafungua:
- Hukum yao kabisa
- Miaka saba ikafika
- Wote watafunguliwa.
- Wakapakiwa sitima ingine
- Na kwao wasikuone
309-315
- Wakawa kama wagane,
- Tanga wakasikilia.
- Wakatiwa katika kazi ya gari
- Kufanyiza hawajui
- Wahindi wanaolia.
- Msimamizi tayari
- Yupo kuwapokea
316-322
- Machozi hujifutia
- Kazi wakifanyia:
- Leo mnajuta nini,
- Baa la kujitakia
- Qadi tamati sha'ri
- Nimesha kuwapa khabari
- Ya Kilwa iliyojiri
323-330
- Yote nimeidhukuri
- Sina nililoacha
- Kwa khabari ya Makunganya
- Kauwawa kimya-kimya
- Fitina hapana tena
- Kilwa yakutokea.
- Nimefikiri peke yangu
- Hatoa rohoni kwangu,
331-338
- Mimi na bibi yangu
- Nyumbani tumejikalia:
- Nilipo nikiandika
- Bibi yangu anapika
- Hatta halafu kikesha
- Chakula, tukajilia,
- Yote nimeyandikia.
- Wakatabahu harufu
339-343
- Wakatabahu: kuandika
- Ushairi umekwisha
- Khabari ya Makunganya
- Iliyo kujiri Kilwa
- Nimekwisha kwambia.
344-348
- Mwenyi kuandika usha'iri
- Ana mu'alimu Mzee
- Bin mu'allimu Ali
- Bin Kidogo bin Al-Qadiri
- Na il usuli Zingibari.