Swahili Tales/Uza ghali, si uza rakhisi

Swahili Tales (1870)
by Edward Steere
Uza ghali, si uza rakhisi
134706Swahili TalesUza ghali, si uza rakhisi1870Edward Steere
[ 296 ]

UZA GHALI, SI UZA RAKHISI.


Aliondoka tajiri mkubwa mwenyi mali mengi, naye waziri wa Sultani. Akakaa katika ulimwengu wake, akazaa kijana kimoja. Na kijana kile, jina lake Ali. Hatta mtoto alipopata mwaka wa khamsi u asherini, babaye akafa. Akasalia yeye na mamaye.

Akarithi mali yake Ali, akatumia mali sana. Hatta Ali akafilisika, akawa maskini thalili pasiwe mtu mmoja amjuaye katika mji ule, rafiki zake yeye, wala wa babaye. Akawa mtu kijana, akatembea katika mji.

Killa amwonaye Ali humwuliza, mali yako waliyatendani, Ali, hatta ukafilisika upesi? Kwani babayo aliacha mali mengi, ungekuwa na akili Ali, mali yako ungedumu nayo. Ali akanena, asiojua maana, haambiwi maana.

Ikawa kazi, neno lake, killa amwulizao humwambia—asiyojua maana, haambiwi maana. Hatta yale maneno mji mzima watu wamejua, kamma Ali, akimwuliza—mali yako umeyatendani, hukujibu, asiyojua maana, haambiwi maana.

Hatta maneno yakafika kwa Sultani. Watu [ 298 ]wakamwambia Sultani, yule kijana wa waziri wako, Ali, amefilisika, watu wakimwuliza—mali yako, Ali, waliyatendani hatta yakaisha upesi? Mali yako ni mengi aliokuachia marehemu babayo, kwani mali yake, ungekuwa na akili, Ali, yangedumu nawe, kwa yale mali kwa kuwa mengi. Na Ali hujibu, akamwambia amwulizaye—asiojua maana, haambiwi maana.

Sultani akanena, kaniitieni Ali, aje ni'mulize maneno haya kweli wanaonena watu ao wanamsingizia. Akaondoka kathi akanena, naam, kweli, Sultani, maneno haya. Akatuma asikari kwenda kumwita kuja wakati wa baraza, na watu pia walipo katika baraza ya Sultani waje, wasikie, maneno haya anaonena Ali kweli ao uwongo.

Hatta Ali akaenda akaazima kanzu mbovumbovu kwa mtu maskini, kwani hapana mtu anayomwamini kumpa nguo zake, na hiyo kanzu Ali apata kwa tafáthali na kwa angukia.

Hatta akaenda mwangoni mwa Sultani, na baraza imejaa tele watu, na Sultani amekaa kitako. Sultani akaondoka, akamwita—Ali! Akaitika—Lebeka. Akamwambia, Ali, nimesikia maneno kama mali yako yamefilisika, na wewe huwajibu watu wanaokuuliza, huwaambia—Asiyojua maana, haambiwi maana.

Akamwambia—Na'am Bwana, mali haya naliyapiga mafungu manne, fungu moja nalitia baharini, fungu moja nalipiga moto, fungu moja nalikopesha wala sitalipwa, fungu moja nimelipa deni wala sijaisha kulipa.

Sultani akamwambia—Ali, uza ghali, si uza rakhisi. Ali akamwambia—Ee Walla, hababi. Akatoka, akaenda zake.

[ 300 ]Akaondoka waziri wake Sultani palepale, katika baraza, akamwambia—Seyedina, maneno haya nayajua maana yake. Sultani akamjibu, akamwambia, kamma wee uyajuapo maneno haya maana zake, billa kumwuliza Ali, uyajue kwa akili yako, mimi Sultani ntakupa usultani wangu, kinachosema na kisichosema katika milki yangu, mimi Sultani nimekupa, yako. Na wewe usipojua maneno haya maana zake kwa akili yako, mali yako nitatwaa yote, wallakini usimwulize Ali.

Akanena waziri, nisipojua maneno haya kwa akili zangu, mimi waziri katika milki yangu nimekupa, Sultani, kinenacho na kisichonena, illa mke wangu mtoto wa watu enda kwao, na kitwa changu halali yako, Sultani.

Sultani akanena, na mimi ntashuka katika ufaume niwe ndiye waziri wako, mimi Sultani.

Akaondoka waziri, akaenda hatta nyumba yake, akanama, akafikiri, akaenda akatwaa vyuo viliomo jamii ndani ya nyumba yake. Akavifunua kutazama maana ya maneno ya Ali, asipate kimoja kilichomo maneno ya Ali. Bassi akakaa kitako akifikiri na kuaza—mimi nimenena kwa Sultani, maneno haya ntayajua kwa akili zangu, nami nimetafakari na kuwaza sikuyajua.

Akamwita, Juma! yule kijana Ali anakaa wapi? Akamwambia, Bwana, Ali gani?

Akamwambia, kile kijana aliokuwa na mali mengi, kijana cha waziri marehemu Hassan, aliofilisika humjui anakokaa? Tafáthali unipeleke, nna maneno naye kutaka kumwuliza. Na maneno haya nimekwambia wewe, usimwambie mtu tena. Nami nimekuacha huru kwa sababu maneno haya asijue mtu.

[ 302 ]Akamwambia—Ee Walla! Ee Walla! namjua anakokaa. Kule-e-e mwisho wa mji, kuna kipenu kidogo karibu na pwani, ndiko anakokaa kwa yule masikini mwenyi chongo anayopita akiomba, ndiye rafiki yake, ndiko anakokaa, hana pahali pangine.

Akaondoka waziri usiku, saa ya sita, watu pia wamelala, yeye na mtumwa wake mmoja, huyu mtumwa ndiye msiri wake, wakaenenda hatta wakafika. Akabisha yule waziri katika kile kipenu, akamwita—Ali! Ali! Akaogopa, asiitike. Akamwambia—Ali!

Akamwambia rafiki yake, amka, amka. Akamwuliza, kuna nini? Akamwambia, kumepiga mtu kibandani kwetu, nami nataajabu usiku huu, huyu mtu mlevi, ao mtu atakayokuja kwiba huku ndani? Lakini sisi fukara, hatuna kitu. Labuda mtu ataka kutuhusudu, kututoa roho zetu. Akamwambia, lakini mimi, na tukae kitako kwanza tusikilize, hatta atakapobisha mwango huu marra ya tatu tumwitikie, hwenda tukamjua sauti yake.

Akamwambia, gissi gani wewe, Ali, kuwa mjinga? Mtu amekuja usiku wa manane, hatumjui atokako, na sisi hatuna kawaida ya kuja mtu kubisha mwango kwetu, ataka nini mtu huyu, isipokuwa labuda ana mambo matatu ataka kwetu, kama Muungu amenijalia mambo haya nayawaza mimi katika roho yangu, ni lile apendalo Mwenyi ezi Muungu.

Akamwambia Ali—Gissi gani, rafiki yangu, maana ya tatu gani haya, unayowaza wewe katika roho yako? Nambie nami najue, tupate kujua sote. Nambia la kwanza.

Akamwambia, la kwanza, ataka kuja kwiba; la pili, ataka kuja kutuua; la tatu, labuda anasema huku kuna mke wake, ao mtumwa wake mwanamke. Ndiyo ninayoyawaza [ 304 ]mimi katika roho yangu. Akamwambia, sijui, rafiki yangu, linalokuja kwa Muungu lote jema.

Ali akasema, akibisha sasa nitamwitikia, akiniua na aniue, akiniacha bass, wala sina buddi illa kumwitikia.

Akabisha waziri, akamwita—Ali! Akamwitikia, lebeka, nani weye unayokuja niita usiku, na usiku huu umekuwa wa manane? Akamwambia, ni mimi, nina shughuli nawe. Akamwambia, sikujui weye, bwana, uliokuja. Akamwambia, usiogope, nimekuja kwita kwa kheri, sikuja kwita kwa shari. Akamwambia, bwana, kuniita kwako, ndiko unisaburi hatta assubui. Waziri akamwambia, hapa nilipo, siwezi kukusaburi hatta kwa dakika moja, hivyo unavyonena ndani naona unakawia. Tafáthali, Ali, toka nje, usikie neno langu nalikwitia.

Akamwambia—Ee Walla, bwana, naweka sikio langu katika mwango uniambie jina lako, ndiyo nitakapoamini kutoka, kwani ndipo nimekwisha kukujua.

Akaenda waziri akamwambia, ni mimi, Waziri wa Sultani, tafáthali toka, nna maneno nawe kwambia na maneno haya kwa faragha. Ee Walla, bwana wangu. Akaenda Ali akamwambia rafiki yake, yule maskini, nimekuja kwitwa na waziri wa Sultani, akataaye witwa hukataa aitiwalo.

Akamwambia, rafiki yangu enenda, labuda kuna kheri nawe. Akifungua mwango Ali akimwona waziri na mtumwa wake mmoja. Akamwambia, Bwana, masalkheiri. Akamwambia, marahaba, Ali, tuondoke, twende zetu kwangu. Akamwambia—Ee Walla, Bwana.

Yule waziri na Ali wakafuatana hatta nyumbani kwake. Waziri akipanda darini, saa saba ikipiga ya usiku, Waziri akamwita mjakazi wake, Mrashi! [ 306 ]Akaitika, lebeka. Kamwambie bibi afanye chakula kwa upesi, kabla saa ya nane hajapiga, na wewe regea.

Alipokuja Mrashi, akamwambia, nimekuja, Bwana. Akamwambia, Mrashi, ukafungue kasha, lete kitambi kimoja cha kilemba, ulete na kofia moja nyeupe ya darizi, lete na kanzu moja ya khuzurungi, ulete na kikoi kimoja seyedia ya uzi, na zote nimefunga pamoja katika bahasha ya leso nyekundu, upesi ulete.

Akaondoka waziri akamwambia Ali, nimekwitia kheri, tafáthali maneno yangu haya asijue mtu, weka ndani nafsi yako. Ali akamwambia, Ee Walla, Bwana, mimi maneno yako nayaweza kuyatoa, Bwana?

Akamwambia, nataka, Ali, unipe maana ya maneno yale waliyomwambia Sultani, unipe na maneno aliokujibu Sultani.

Akamwambia, Sultani ameniambia, Uza ghali, si uza rakhisi.

Ali, Ali, utafáthali ukanambie maneno haya, utanambiaje, na Sultani ameniambia, uza ghali, si uza rakhisi? Ntakupa shamba langu.

Akamwambia, Sultani ameniambia, uza ghali si uza rakhisi.

Akamwambia, Ali, bokhari zangu zote twaa zilio mjini.

Ali akanena, Sultani ameniambia, uza ghali si uza rakhisi.

Waziri akanena, Ali, twaa yote mashamba yangu.

Ali akanena, Sultani ameniambia, uza ghali si uza rakhisi.

Waziri akamwambia, twaa yote milki yangu.

Ali akanena, Sultani ameniambia, uza ghali si uza rakhisi.

Waziri akamwambia, twaa kisemacho na kisichosema katika milki yangu mimi waziri, nami nambie maneno haya.

[ 308 ]Ali akanena, Sultani ameniambia uza ghali si uza rakhisi.

Akaondoka waziri, akamwambia, ntakupa nyumba yangu yote nnaokaa na mali yaliomo yote, illa mke mwana wa watu enda kwao.

Akamwambia, bassi sasa niandikie khati ya mkono wako.

Waziri akamwita Mrashi. Akamwitikia, lebeka, Bwana. Akamwambia, lete kalamu na wino na karatasi kishubakani. Mrashi akaenda akaleta. Waziri akakamata karatasi na wino, akamwandikia Ali, nimempa yote milki yangu kinenacho na kisichonena, hatta nyumba yangu nikaao mwenyewe, illa mke mwana wa watu enda kwao. Akatwaa khati waziri akampa Ali.

Imekuwa saa ya kumi, tuondoke tukasali kwanza, kuregea kwetii kusali nikupe maana zako unazozitaka.

Wakashuka wakaenda zao kusali, wakarudi mosketini. Akawambia, haya, Ali, nambie, kwani tena kumekucha.

Ali akamwambia, maana ya kunena, asiojua maana haambiwi maana, kwa sababu nikimweleza mtu asiokuwa na akili hatajua. Ndio maana killa aniulizaye nikimwambia—asiojua maana haambiwi maana. Na Sultani aliponiita akaniuliza hayaambiwi, kwani Sultani ana akili. Naye, ndiyo akanijibu—Uza ghali, si uza rakhisi. Haya maneno yako.

Bassi nieleze mali haya yalipotea.

Ali akanena, mali haya naliyapiga mafungu manne, [ 310 ]fungu moja nalitia baharini, funga moja nalipiga moto, fungu moja nalikopesha wala sitalipwa, fungu moja nimelipa deni wala sijaisha kulipa.

Bassi, nambie, Ali, maana ya kutosa baharini fungu moja, maana yake nini?

Ali akamwambia waziri, niwie rathi kwa killa nitakalonena stahamili. Akamwambia, baharini ni mali naliyokwenda kufanya usherati na waanaake, yamepotea mali yale sitayapata tena, bassi kama naliyotia baharini, kwani kitu kikizama bahari hakipatikani.

Na maana ya kupiga moto fungu moja?

Ali akanena, nalikula sana, nalivaa sana, nalitumia sana, ndiyo maana ya kupiga moto, kwani havitaregea tena katika mikono yangu.

Nambie fungu la tatu, maana ya kukopeshwa wala hutalipwa nini?

Akamwambia waziri, ni kama mtu waliompa mkeo mahari yake, haitarudi tena, bassi ndio maana ya kukwambia nimekopesha wala sitalipwa.

Akamwambia, fungu la nne nambie maana yake ya kunena umelipa deni wala hujaisha kulipa.

Akamwambia waziri, ni kama mtu aliompa mama yake mali kutaka kumfurahisha roho yake, walakini mimi mtoto sijui kama mama yangu nifurahi roho yake kwa haya naliyomtendea, bassi na mimi kijana hunena rohoni mwangu, hajaisha mama yangu kufurahi kwa yale naliompa mali. Ndio maana ya kukwambia, nimelipa wala sijaisha kulipa.

Akamwambia, ahsánt, Ali, na maneno yako nimeyasikia.

Nao kumekuwa jua lachomoza, saa kumi na mbili zimekwisha piga. Akakaa waziri na roho yako furaha, [ 312 ]nitakwenda leo kupata usultani, kwani nimeyajua kwa akili yangu. Akakaa waziri hatta saa ya tatu Sultani amebarizi. Akitoka nyumbani mwake waziri hana kitu illa kanzu yake moja ilio mwilini mwake. Akatoka na furaha roho yake.

Akaenda hatta akafika mbele ya mwango wa Sultani. Watu waliopo na asikari jamii waliopo wakastaajabu. Ah! Waziri mkubwa, ndiye mwenyi mambo yote ya Sultani, anakuja kwa kanzu moja, hatta viatu miguuni hana. Hatta watu wanamtaajabu pasiwe mtu mmoja aliojua alionalo katika roho yake. Wale watu wajinga wakanena, labuda anafiwa na mkewe. Ndiye akaja vile kwa Sultani.

Akaondoka waziri, akamwambia, Subalkheiri Seyedina. Sultani akamwambia, Allah bilkheir al wazir, karib. Akakaa kitako.

Sultani akanena, nambie khabari zako, walizonazo. Akamwambia, khabari kheri, nimekuja kukupa maana ya maneno yako yale twalioahadiana mimi nawe, Sultani. Nami nimeyajua kwa akili zangu, Sultani.

Sultani akamwambia, nieleze la kwanza.

Akamwambia, yule Ali walipo watu waka'muliza, kwani mali yake yakafilisika, kuwaambia, asiojua maana haambiwi maana, kwa sababu wale watu wajinga hatawaambia maneno yale. Hawajui la kumjibu, bassi si afathali hawaambii wasiojua maana? Kwani mwenyi kumwambia mtu neno ataka kujibiwa. Utamwambia mtu neno hajui la kujibu? Bassi ndio maana yako asiwaambie. Sultani [ 314 ]akanena, na'am, inna kweli maneno haya. Akamwambia, nipe maana, waziri, ya mafungu manne haya.

Akamwambia, la kwanza, Sultani, lilitoswa baharini fungu moja, na moja lalipigwa moto, na moja lalikopeshwa wala hatalipwa, na moja amelipa wala hajaisha kulipa.

Akamwambia, na'am waziri, inna maneno yako kweli. Akamwambia, nipe maana ya kutoswa baharini fungu moja hili.

Akamwambia, ni mali aliotwaa Ali akaenda kufanya uasherati nje, mali yale yakapotea, ndiyo maana ya kuambiwa, fungu moja lile limeingia baharini.

Akamwambia, na'am waziri, inna neno hili kweli. Sultani akanena, hii fetha kwisha kupeleka waanawake fetha haipatikani tena, kweli maneno yake, kama imeingia baharini. Nipe na maana ya fungu la pili liliopigwa moto, nipe maana yake.

Akanena waziri, Ali alikula sana, alivaa sana, alitumia sana, ndiyo maana ya kupigwa moto mali zile, hazitaregea tena mkononi mwake.

Sultani akanena, na'am inna kweli maneno haya, waziri, kwani hii mali ukiisha kununua chakula, ukanunua na nguo njema, ukavaa, imekwisha potea mali hairudi. Maneno yake amenena kweli Ali, kama fungu hili limepigwa moto. Akamwambia, nambie, waziri, katika fungu la tatu maana yake.

Waziri akanena, fungu la tatu amelikopesha, wala hatalipwa. Akamwambia, maana yake nini ya kukopesha mali hayo wala hatalipwa? Waziri akanena, ni mali aliyetoa kumpelekea mahari yake manamke, utapomwacha, [ 316 ]mali yako hakurudishii, ndio maana, akanena, nimekopesha sitalipwa.

Akamwambia, na'am waziri, inna maneno haya kweli. Sultani akanena, mwenyi kumpa manamke mahari hapati tena, utakapokuwa manamume amefilisika, hafanyi roho yake njema yule manamke kukupa. Kwani umekuwa masikini, akuona kama mjinga, hakujui kama aliokuwa mume wangu, kwani mnekuwa fukara, tena umekuwa mbaya, tena amekufanya mtu mjinga, kwani umekosa mali. Kwani walipokuwa na mali walikuwa manamume mzuri, walikuwa kijana una akili, walionekana kama kijana cha Sultani.

Akaondoka waziri akanena, kweli, Sultani, mtu akikosa mali hawi mtu mbele za watu. Sultani akanena—Waziri, nambie maana ya fungu la nue, kulipa wala hajaisha kulipa.

Akamwambia Sultani, maana yake, Ali alitoa mali katika fungu moja akampa mamaye. Bassi Ali hajui kama mamaye roho yake i rathi kwa mali aliyopewa na mwanawe. Bassi Ali ananena, labuda mama yangu hajafurahi kwa lile nalilomtendea, ndio maana ya kunena Ali, kulipa wala sijaisha kulipa.

Sultani akamwambia, na'am waziri. Akaondoka kitini akasimama, na baraza imejaa tele watu, akamwita akida, akamwambia, nenda gerezani kamwamuru jemadari apige goma, sasa amekuwa Sultani waziri wangu, na mimi ndiye nimekuwa waziri wake; na ninyi jamii asikari, na jamii ya walio mliomo katika mji, Waarabu, na Waswahili, na jamii Wangazidja, mtiini Sultani.

Akiondoka, akautwaa usultani waziri. Bass, wakakaa kitako mda wa siku mbili.

[ 318 ]Mtu akipita kwa nyumba iliokuwa ya waziri amkuta Ali katika dirisha, anachungulia anamwamru mchunga kutandika frasi, ataka kwenda kutembea. Yule Mwarabu akamwita, Ali! Akamwitikia, na'am. Mbona u katika nyumba hii? Ali akamwambia, Sultani hakuniambia, uza ghali si uza rakhisi, ati? Nami nimekuza ghali.

Ahh! Yule Mwarabu akataajabu, gissi gani huyu Ali kuwa katika nyumba ya waziri mkubwa, lakini haithuru. Akakaa.

Akapita Mwarabu mgine akamkuta chini sebulani, akamwita, Ali! Akamwitikia, na'am. Akamwambia, mbona nakuona hapa, Ali? Akamwambia, hii si nyumba yangu? Gissi gani kuwa hii nyumba yako? Sultani ameniambia, uza ghali si uza rakhisi, nami nimekuza ghali ati.

Akaondoka yule Mwarabu, akaenenda hatta mwangoni kwa Sultani. Akamwambia, bwana wangu, seyedi yangu, nimekuta mtumwa wako, Ali, katika nyumba ya waziri wako, nikamwuliza—Ali! Akaitika, na'am. Unafanyaje katika nyumba hii wewe? Ali akanijibu, Sultani ameniambia, uza ghali si uza rakhisi, nami nimekuza ghali.

Yule Sultani akataajabu, ndio mambo alionitenda waziri, nami naye twalipana wahadi wa kutosha kumwuliza Ali, kumbe yeye amekwenda kumwuliza Ali, na mali yake kufilisika? Bassi sasa mbona amekosa kuwili, amekosa mali yake, amekosa na usultani. Na weye upesi enenda kamwita Ali aje. Ee Walla, Bwana.

Akitoka mbio kwenenda akamkuta Ali, ataka kuingia mashuani kwenda kutembea. Akamwita, Ali! Akamwambia, na'am. Akamwambia, upesi, unakwitwa kwa [ 320 ]Sultani. Ali akanena, Ee Walla, ni kama Sultani, Sultani wangu.

Akaondoka Ali akapanda darini, akamwita—Mrashi, nitezamie katika nguo njema ziliomo katika makasha, kwani wewe ndiye ujuaye zayidi kuliko mgine. Akaenda Mrashi akifungua kasha akitoa joho mzuri, akatoa kilemba kizuri, akatoa na deuli aali akatoa na janvia moja la temsi la thahabu, akatoa na kitara kimoja cha albunsayidi cha Arabu, akatoa na kitupa cha hal wáradi Stambuli, akampelekea bwana.

Alipoziona Ali nguo zile akafurahi, akatwaa, akavaa, akishuka na yule Mwarabu, wakaenenda hatta wakafika katika mwango wa Sultani. Wakamwambia, pita sebulani. Akapita, akakaa kitako.

Akishuka yule Sultani kuja chini kubarizi, akashuka na yule aliokuwa Sultani kwanza, sasa aliokuwa waziri. Akamwambia waziri, akaitika, na'am. Akamwuliza, zile sharti zetu hazikufaa, nalikwambia mimi sharti zangu ujue kwa akili yako usiende kumwuliza Ali? Akamwambia, naam. Na wewe ukazunguka, ukaenda kumwuliza Ali. Akamwambia Sultani, sikumwuliza Ali. Sultani akanena, Ah! Ali si huyu yuko? Akamwambia, tumwite, aje mbele zako tupate kusadiki kama maneno haya kuyajua kwa akili yako wewe, ila kwa Ali kukwambia. Akamwambia, na'am, mwita Ali aje.

Akaondoka Sultani, akamwita Ali. Akamwambia, lebeka, hababi. Akamwambia, njoo. Akamwambia, gissi gani wewe, Ali, kwenda kukaa katika nyumba ya waziri, una maana gani? Akamwambia, na'am, Sultani, [ 322 ]waliniambia wewe, uza ghali si uza rakhisi, na khati ya waziri hii alioniandikia, nawe soma, Sultani, ujue mambo haya kweli.

Sultani akaishika akaisoma khati, akamwambia, kweli, Ali, umekuza ghali hukuza rakhisi.

Akaondoka Sultani akamwita waziri. Akamwambia, lebeka hababi. Akawaambia watu, mlioko katika baraza, mkubwa na mdogo, na Banyani, na Mwarabu, na Msheheri, na Mngazidja, na Mswahili, na jamii ya watu waliomo katika inchi—bassi mimi nimemwondoa, hamo katika uwaziri wala katika usultani, hali yake kaiua hali ya waliyo katika mji. Na sasa huyu Ali ndiye amekuwa waziri wangu mkubwa, killa mtu atakalo, akiwa mume, akiwa mke, akiwa Mwarabu, akiwa Mzungu, wote na waende kwa Ali ndio atakokwisha mambo yenu.

Na hii hadithi imetokana na Ninga.