Swahili Tales/Hadithi ya Liongo

135169Swahili TalesHadithi ya Liongo1870Edward Steere
[ 440 ]

HADITHI YA LIONGO.


Hapo zamani za Shanga palikuwa mtu, jina lake Liongo, naye ana nguvu saaa, mtu mkubwa sana katika mji. Akauthi mno watu, hatta siku hiyo, wakafanya shauri kumwendea nyumbani kwake kumfunga. Wakaenda watu wengi sana wakamingilia nyumbani gháfula, wakamkamata wakamfunga, wakaenda naye hatta gerezani, wakamtia.

Akakaa siku nyingi, akafanya hila hatta kufungua. Akatoka nje, akauthi watu vilevile, siku nyingi. Watu hawawezi kwenda mashamba, wala kukata kuni, wala kuteka maji. Wakauthika sana.

Watu wakasema, tufanye hila gani, hatta tumpate, tumwue? Akanena mmoja, tumwendee anapolala, tuniwulie mbali. Wakasema wangine, mkimpata, mfungeni, mmlete. Wakaenda wakafanya hila, hatta wakampata, wakamfunga, wakamchukua mjini. Wakaenda wakamfunga mnyororo, na pingu, na mti kati.

Wakamwacha siku nyingi, mamaye humpelekea kula kulla siku. Na mbele ya mlango kule alikofungwa, wamewekwa asikari wanayomngojea, hawaondoki marra moja ela kwa zamu.

Siku nyingi na miezi mingi imepita. Kulla siku, [ 442 ]usiku usiku, kuimba nyimbo nzuri, kulla asikiaye huzipenda sana zile nyimbo. Kulla mtu humwambia rafiki yake, twende tukasikilize nyimbo za Liongo, anazokwimba chumbani. Huenenda, wakisikiliza. Kulla siku ikipata usiku, huenda watu, wakamwambia, tumekuja kwimba nyimbo zako, tusikie. Huimba, hawezi kukataa, wakazipenda mno watu mjini. Na kulla siku kutunga nyingine nyingine kwa sikitiko la kufungwa. Hatta watu wamezijua nyimbo zile kidogo kidogo, lakini yeye, na mamaye, na mtumwa wake wanazijua sana. Na maana yake zile nyimbo mamaye azijua, na wale watu mjini hawajui maana yake.

Hatta siku hiyo kijakazi chao ameleta chakula wakamnyang'anya wale asikari, wakala, wakamsazia makombo, wakampa. Yule kijakazi akamwambia bwana wake, nimeleta chakula, wameninyang'anya hawa asikari, wamekula, wamesaza haya makombo. Akamwambia, nipe. Akapokea, akala, akashukuru Muungu kwa yale yaliompata.

Akamwambia kijakazi chake (na yeye ndani na kijakazi yu nje ya mlango)

Ewe kijakazi nakutuma uwatumika,
Kamwambia mama, ni mwinga siyalimka.
Afanye mkate, pale kati tupa kaweka,
Nikeze pingu na minyoo ikinyoka,
Ningie ondoni ninyinyirike ja mana nyoka,
Tatange madari na makuta kuno kimeta.

Maana yake—Wee kijakazi utatumika kamwambia mama, ni mjinga sijaerevuka, afanye mkate, katikati aweke tupa nikate pingu, na minyololo ikifunguka, niingie njiani, [ 444 ]niteleze kama nyoka, nipande madari na kuta, nikitezama huko na huko.

Akamwambia, salaam sana mama, mwambie kama haya niliokwambia. Akaenda, akamwambia mamaye, akamwambia, salaam sana mwanao, ameniambia maneno kuja kukwambia. Akamwambia, maneno gani? Akamwambia, kama yale yalioambiwa.

Mamaye akajua, akaenda zake dukani, akabadili mtama, akampa mtumwa wake kutwanga. Yeye akaenda kununua tupa nyingi, akaleta. Akatwaa unga ule, akafanya mikate mizuri mingi. Akatwaa chachu, akafanya mkate mkubwa, akatwaa tupa akatia ndani, akampa mtumwa wake, kumpelekea.

Akaenda nao, akifilia mlangoni asikari wakamnyang'anya, wakachegua mikate mizuri, wakala wao. Ule wa chachu wakamwambia, mpelekea bwana wako. Yule akampelekea, akauvunja, akatoa tupa zile akaziweka, akala mkate huu akanywa maji, akashukuru Muungu.

Na wale watu mjini wataka auawe. Mwenyewe akasikia ya kuwa ya kwamba utauawa. Akawaambia asikari, nitauawa lini? Wakamwambia, kesho. Akawaambia, kanitieni mama yangu na mwenyi mji, na watu mjini wote, nije niagane nao.

Wakaenda, wakawaita, wakaja watu wengi wote, na mama yake na yule mtumwa wake.

Akawauliza, mmekutanika nyote? Wakamjibu, tumekutanika. Akawaambia, nataka pembe, na matoazi, na upato, zikaenda zikatwaliwa. Akawaambia, nna machezo leo nataka kuagana nanyi. Wakamwambia, vema, haya, [ 446 ]pige. Akawaambia, mmoja ashike pembe, na mmoja ashike matoazi, na mmoja ashike upato. Wakamwambia, tupigeje? Akawafundisha kupiga, wakapiga.

Naye mwenyewe ndani kule aliko akaimba, hatta ilipositawi ngoma, akashika tupa, akakata pingu. Ile ngoma ikinyamaa naye bunyamaa, akaimba, wakipiga, yeye akakata pingu.

Na watu wale hawana khabari ilioko ndani, hatta ikakatika pingu, akakata na mnyororo hatta ukakatika. Na wale watu hawana khabari kwa shanko ya ngoma. Wakitahamaka amevunja mlango amewatokea nje. Wakitupa vitu hivi kwenda mbio wasidiriki, akawakamata akawapiga vitwa kwa vitwa akiwaua. Akitokea nje ya mji, akaagana na mamaye, kutuonana tena.

Akaenda zake mwituni akakaa kitako siku nyingi huuthi watu vilevile na kuwaua watu.

Wakatuma watu wa hila, wakawaambia, enendi, mkafanya rafiki hatta mmwue. Wale wakaenda wa khofu. Walipofika wakafanya urafiki, Hatta siku hiyo wakamwambia, tule kikoa, Sultani. Yeye Liongo akawajibu—

Hila kikoa halipani nikatamno?

Maana yake—Nikila kikoa nitalipa nini, masikini mno? Wakamwambia, tule kikoa cha makoma. Akawauliza, tutakulaje? Wakamwambia, atapanda mtu mmoja juu ya [ 448 ]mkoma akaangue, tule, tukiisha apande mgine, hatta tuishe. Akawaambia, vema.

Akapanda wa kwanza, wakala. Akapanda wa pili, wakala. Akapanda wa tatu, wakala. Na wale wamefanya hila, atakapopanda Liongo tumpige kwa mishare kulekule juu.

Liongo akatambua kwa akili yake. Hatta walipokwisha wote, wakamwambia, haya, zamu yako. Akawaambia, vema. Akashika mkononi uta wake na viembe, akawaambia—

Tafuma wivu la angania, tule cha yayi.

Maana yake, Nitapiga bivu la juu tule cha kati. Akapiga, likakatika tawi, akapiga tena, likakatika la pili, akaupukusa mkoma mzima, yakajaa tele chini. Wakala. Hatta walipokwisha, wale watu wakasema wao kwa wao, ametambua huyu, sasa tufanyeje? Wakanena, twendeni zetu. Wale wakamwaga, wakamwambia—

Kukuingia hadaani Liongo fumo si mtu,
Yunga jini Liongo okoka.

Maana yake, Hukuingia ujingani, Liongo mfalme, wewe si mtu, kamma Sheitani umeokoka.

Wakaenda zao, wakajibu kwa yule mkuu wao, alioko mjini, wakamwambia, hatukuweza.

Wakafanya mashauri—nani atakayeweza ku'mua? Wakanena, labuda mtoto wa nduguye. "Wakaenda wakamwita. Akaja. Wakamwambia, enenda, kamwuliza babayo, kitu gani kinachomwua, ukiisha kujua, uje [ 450 ]utwambie, na akiisha kufa tutakupa ufaume. Akawajibu, vema.

Akaenda. Alipofika akamkaribisha, akamwambia, umekuja fanya nini? Akamwambia, nimekuja kukutazama. Akamwambia, najua mimi umekuja kuniua, na hao wamekudanganya.

Akamwuliza, baba, kitu gani kinachokuua? Akamwambia, sindano ya shaba, mtu akinichoma ya kitovu, hufa.

Akaenda zake mjini, akawajibu, akawaambia, sindano ya shaba ndio itakayo'mua. Wakampa siudano, akarudi hatta kwa babaye. Alipomwona, akaimba yule babaye, akamwambia—

Mimi muyi ndimi mwe mao, situe
Si mbwenge mimi muyi ndimi mwe mao.

Maana yake, Mimi mbaya ndiye mwema wako, si nifanya mbaya, mimi ndimi mbaya ndiye mwema wako. Akamkaribisha, akajua, huyu amekuja kuniua.

Akakaa siku mbili, hatta siku hiyo usiku amelala, akamchoma sindano ya kitovu. Akaamka kwa uchungu wake, alishika uta wake na viembe, akaenda hatta karibia visima. Akapiga magote, akajitega na uta wake. Akafa palepale.

Hatta assubui, watu wanaokuja teka maji wakamwona, wakamthani mzima, wakarudi mbio. Wakatoa khabari mjini, leo maji hayapatikani. Kulla endaye hurudi mbio. Wakatoka watu wengi wakaenda, wakifika, walipomwona wasiweze kukaribia, wakarudi. Siku tatu watu wanathii kwa maji, kuyakosa.

[ 452 ]Wakamwita mamaye, wakamwambia, enenda kasema naye mwanao, aondoke, tupate maji, ao tutakuua wewe.

Akaenda hatta alipofika akamshika mwanawe kumtumbuiza kwa nyimbo, akaanguka. Mamaye akalia, akajua mwanawe amekufa.

Akaenda kuwaambia watu mjini, ya kwamba amekufa, wakaenda kumtezama, wakamwona amekufa, wakamzika, na kaburi lake laonekana katika Ozi hatta leo.

Wakamkamata kile kijana, waka'mua, wasimpe ufaume.